UGUMU ULIOPO KATIKA KUFASILI MAANA YA NENO
Neno ni dhana iliyojadiliwa na wanaisimu kadhaa ambao walijadili katika namna tofauti, utofauti huo umesababishwa na vigezo walivyovitumia. Kuna waliolichambua neno kwa kigezo cha kifonolojia, kisemantiki, kiotografia, kisintaksia, kileksika na vigezo vinginevyo. Insha hii itajadili maana ya neno kwa vigezo hivyo (vilivyotajwa hapo juu), kuonyesha ubora au upungufu, kuonyesha ugumu wa kifasili dhana hiyo na mwisho kuhitimisha.
ST. FRANCIS MAUA SEMINARY
Kifonolojia, neno ni silabi au mkusanyiko wa silabi zinazotamkwa au kuandikwa (TUKI, 1990), silabi hizo huwa ni tofauti kutoka lugha moja hadi nyingine. Mfano katika Kiswahili neno “karibu” lina silabi tatu (3)
$ ka $ $ ri $ $ bu $.
Kwa kigezo hiki pia, neno huwezea kufafanuliwa kama vipande vya matamshi yaani fonimu zinazopangwa katika mpangilio maalum ili zilete maana.
Mfano neno “bata” lina fonimu nne ambazo ni /b/, /a/, /t/, /a/
Mpangilio huu ukigeuzwa maana ya neno hupokea na watumiaji wa lugha hiyo hawataelewa maana yake.Mfano neno*taba, japokuwa limeundwa na fonimu zilezile halina maana kwa sababu mpangilio huo haupo katika lugha hiyo.
Vilevile kwa mujibu wa mtandao (Taz. www.sussex.ac.....), katika lugha ya Kiingereza sifa itumikayo kuonyesha kuwa hili ni neno ni mkazo msingi ambao huwa ni mmoja tu katika neno.
Mfano:Juma is going to school.
Tungo hii ina maneno matatu “Jumas’ “going” na “school”. Kwa kigezo hiki “is” na “to” si maneno.
Pamoja na kigezo hiki kuzingatia sana viambajengo vya lugha kama fonimu, silabi na mkazo bado ina upungufu hasa katika kipengele cha mkazo, kila lugha ina sheria zake katika uwekaji mkazo. Kwa mfano katika Kiswahili. Mkazo msingi huwekwa katika silabi ya mwisho kasoro moja na huhama kwenda katika neno la mwisho kila maneno yanapoongezeka katika tungo.
Mfano
- Anakula.
- Anakula chakula.
-Anakula chakula kitamu.
Silabi iliyopigiwa mstari ina mkazo msingi.
Mfano huo hapo juu unaonyesha kuwa mkazo msingi huhama kwa kadiri maneno yanavyoongezeka.
Vilevile kuna lugha nyingine kama Kihehe, Kidigo, Ci-ruuri hazina mkazo bali zina toni (Massamba; 2010) hivyo kwa kigezo cha mkazo ni vigumu kubaini maneno katika lugha hizo.
Kiotografia, neno limefasiliwa kama mfululizo wa herufi zilizofungamana pamoja na kuzungukwa na nafasi tupo (Mdee, 1997). Utaratibu wa kuweka nafasi hufuata taratibu maalumu za kiotografia ambazo hutofautiana kutegeana na lugha moja na nyingine.Kwa mfano katika lugha ya kiswahili ,
-Mama alirudi jana usiku.
Tungo hii una maneno manne yaani “mama” “alirudi” “jana” na “usiku”
Kwa ujumla ubora wa mkabala huu ni kwamba, husaidia sana uandishi wa matini za kitaaluma hasa kwa lugha zinazofuata utaratibu huu. Lakini vilevile ina upungufu kama ifuatavyo.
Dhana ya nafasi tupu ipo tu kwenye maandishi, tunapozungumza hatuachi nafasi tupu baina ya maneno, tunayatamka yote kwa mfululizo.
Vilevile utaratibu wa kuweka nafasi mwanzoni au mwishoni mwa neno haupo katika lugha zote, kuna lugha kama Kigiriki na kieskimo maneno yake katika tungo hayawekewi nafasi tupu. Kwa mfano tungo hii ya lugha ya Kieskimo “Kaipiallrullinink”yenye maana ya kuwa “wote wawili walikuwa na njaa”. Tungo iliyowekwa katika herufi za italiki ni ya kieskimo ambayo haina nafasikati ya neno moja na lingine.
Pia maneno ambatani yatahesabiwa kuwa ni neno moja au mawili?, (www.sussex.ac.....).Haya ni maneno mawili au zaidi lakini yamebeba dhana moja Kwa mfano katika Kiingereza
- “pocket money”
- “Bus driver”
Katika Kiswahili maneno ambatani ni kama
- Gongo la Mboto
- Kata mbuga.
Sambamba na hayo, upungufu mwingine wa dhana hii ni kwamba, haiangalii viambajengo vinavyojenga neno kwa mfano fonimu silabi, mkazo na toni.
Kwa upande wa semantiki, neno limefasiliwa kipashio kidogo cha lugha chenye maana (Mdee, 1997) kwa maana hiyo neno ni lazima liwe na maana inayoeleweka kwa jamii inayotumia lugha hiyo. Mfano:
Mama – Mzazi wa kike
Ndama – Mtoto wa ng’ombe
Fasili hii ina mashiko kwa sababu maneno mengi katika lugha yana maana na hueleweka kwa watumiaji wa lugha. Lakini kwa aupande wa pili si kila neno linalotumika linaweza kuwa na maana ya wazi au ya kisemantiki,kwa mfano viunganishi kama na, ya, kwa, wakati n.k, ambavyo japokuwa havina maana ya kisemantiki lakini vina uamilifu kisarufi.
Wanataaluma wa kisintaksia wanafasili neno kama kipengele kidogo kabisa cha sentensi ambacho kinaweza kuhamishwa kutoka nafasi moja hadi nyingine bila kuathiri sarufi ya lugha katika tungo/sentensi hiyo. Cruse (1986) akinukuliwa na Mdee (1997). Kwa ujumla hapa kinachotazamwa zaidi ni kategoria za maneno na mpangilio wake katika tungo.
Mfano
- Ali alimuua Ahmad
N T N
- Ahmad alimuua Ali
N T N
Hapa N ni Nomino na T ni kitenzi.
Japo nomino zimebadilishana, lakini sarufi ya lugha hiyo haijaathirika.
Kwa ujumla utaratibu huu unasaidia sana katika kujifunza sarufi ya lugha hasa miundo ya tungo kama virai,vishazi na sentensi na pia hata kujua sehemu za tungo kama kiima na kiarifu.
Lakini kwa upande mwingine kigezo hiki kina upungufu kwa sababu sio maneno yote yanayoweza kuhamishwahamishwa bila kuvuruga sarufi ya lugha.
Kwa mfano.
- Alia amesimama kando ya mto
- Amesimama kando ya mto Ali.
- Kando ya mto Ali amesimama
* Mtoto Ali amesimama kando ya
* Mto ya kando amesimama Ali.
Sentensi mbili za mwisho (zilizowekewa) nyota kwa sababu hazikidhi haja ya usahihi wa kisarufi (Mdee, 1997:7)
Vilevile unapohamisha maneno basi maana ya neno pia hubadilika
Mfano
(i) Zubeda anampenda Zawadi
(ii) Zawadi anampenda Zawadi
Japokuwa nomino katika sentensi hizo zimebadilishana nafasi, haijaathiri sarufi ya lugha lakini kimaana imebadilika kwa sababu katika sentensi (i) Zubeda ndie anatenda tendo na katika sentensi (ii) Zawadi ndio anatenda tendo.
Kileksika, neno ni dhana dhania ya kileksikoni ambayo neno hurejelewa kama Leskimu. Leskimu ni msamiati ulioorodheshwa kwenye kamusi (Katamba, 199:17), neno hili (Leskimu) huwa na maana kimsamiati (TUKI: 1990). Kwa kawaida Leskimu huwa na vibadala vyake kutegemeana na leskimu yenyewe.
Mfano:
go - vibadala vyake ni go, going,went, goes.
cheza - cheze, chezea, mchezea, chazeana, n.k.
refu - refu, ndefu, mrefu, kirefu, n.k.
Japokuwa dhana hii inasaidia sana katika taaluma za mofolojia, leksikografia na taaluma nyinginezo, bado ina mapungufu au haijitoshelezi kwa sababu katika lugha kuna maneno ambayo yakisimama pake yake hayaleti maana na si leskimu katika kamusi lakini maneno hayo yakikurubishwa na maneno ya kileksika huleta maana. Katika Lugha ya Kiswahili kwa mfano kuna viunganishi kama na, ya, kwa n.k na vitenzi vishirikishi (husishi) kama ni, si, -kuwa na ndi- (ndiye, ndio n.k) ambavyo si leskimu lakini hufanya kazi ya kisarufi au vina uamilifu katika lugha.
Kutokana na fasili hizo tunaona kuwa kuna ugumu katika kufasili dhana ya neno, ugumu huo unasababishwa na sababu zifuatazo.
Spencer (1991) anadai kuwa ugumu wa kufasili neno unasababishwa na utofauti wa lugha kimaumbo, kimatamshi, kimuundo na kimaana, hivyo ni vigumu kuhusisha fasili moja inayoweza kuhusisha mifumo yote ya lugha kwa usahihi kwa sababu lugha hutofautiana katika vipengele hivyo.
Naye Mdee (1997) anadai kuwa kufasili neno kuna ugumu, ugumu huo unatokana na mitazamo tofauti ya wanaisimu kuhusu kipashio hicho (neno) kiotografia, kimaumbo na, kimatamshi. Hivyo kwa kuwa kila mwanaisimu anamtazamo wake hivyo hushindwa kukubaliana maana moja ya neno.
Vilevile kwa mujibu wa mtandao (w.w,w. sussex ..) unadai kuwa ugumu wa kufasili neno unasababishwa na utofauti wa utamaduni na mazingira na maarifa ya wanaisimu. Hii ndio sababu kila mtu anafasili neno kutokana na lugha yake ilivyo na maarifa aliyonayo, wanafonolojia wanafasili neno kwa kuzingatia nduni za fonolojia kama silabu, fomimu, toni, mkazo, wanaleksikografia wamefasili neno kama leskimu n.k.
Kwa ujumla tunaweza kuhitimisha kwa kusema kwamba, ugumu wa kufasili neno tofauti za wanaisimu kilugha, kitaaluma, kimazingira kimtazamo na kiutamaduni.Hivyo ili kuondoa au kuziba upungufu wa kigezo kimoja, vigezo zaidi ya kimoja vitumike katika kuangalia maana za maneno katika lugha tofauti.
MAREJEO
Katamba, F. (2993) Morphology. Macmillan Press LTD. London.
Mdee,D. (1997) Nadharia za Leksikografia. TUKI, Dar-es-Salaam.
Spencer, A. (1991) Morphological Theory: An Introduction to Word Stucture in Generative Grammar. Blackwell Publishers. UK.
TUKI (1990) Kamusi sanifu ya Isimu na Lugha. TUKI. Dar-es-Salaam
Maintained by an ICT consultant and Director of Studies: IFF YOU NEED HELP PLZ CALLA US VIA 0782 474941 0767 4749411 OR VIST www.kcckibaha.blogspot.com kcckimisha@gmail.com
No comments:
Post a Comment