Thursday, October 30, 2014

CHIMBUKO - USHAIRI

CHIMBUKO - USHAIRI





CHIMBUKO LA USHAIRI
Dhana ya ushairi imejadiliwa na wataalamu mbalimbali huku kila mmoja akitoa fasili yake. Baadhi ya wataalam hao ni kama ifuatavyo:
Mssamba, (2003) akimnukuu Shaban Robert, anasema; “ushairi ni sanaa ya vina inayopambanuliwa kama nyimbo, mashairi na tenzi zaidi ya kuwa na sanaa ya vina ushairi unaufasaha wa maneno machache au muhtasari.”
Mnyampala (1970) anasema kuwa “ushairi ni msingi wa maneno ya hekima tangu kale ndicho kitu kilichobora sana maongozo ya Dunia kwa kutumia maneno ya mkato na lugha nzito yenye kunata iliyopangwa kwa urari wa mizani na vina maalum.”
Amri Abeid (1954:1) anasema kuwa “ushairi au utenzi ni wimbo, hivyo kama shairi haliimbiki halina maana.”

Encyclopedia American (EA) inaeleza kuwa ushairi ni kauli zenye hisia na ubunifu, mpangilio fulani wenye urari, uwasilishaji wa tajiriba au mawazo ya mtunzi kwa maana ambayo huibua tajiriba kama hiyo katika nyayo za wasomaji au wasikilizaji na kutumia lugha ya picha yenye wizani wa sauti.
Mulokozi na Kahigi (1982:25) wanasema ushairi ni “sanaa inayopambanuliwa kwa mpangilio maalum na fasaha na wenye muwala, kwa lugha ya picha, sitiari au ishara katika usemi, maandishi au mahadhi ya wimbo ili kuleta wazo au mawazo, kufunza au kueleza tukio au hisia fulani kuhusu maisha au mazingira ya binadamu kwa njia inayogusa moyo.”
Hivyo basi tunaweza kusema kuwa ushairi ni kazi ya sanaa yenye kuandikwa au kuimbwa kwa kufuata kanuni za ushairi au kutofuata kanuni za ushairi ikiwa na maana kuwa ushairi waweza kuwa wa kimapokeo au wa kisasa ilimradi ushairi huo uwe na ujumbe.
Dhana ya chimbuko inafasiliwa na TUKI (2004) kuwa ni mwazo au asili ya kitu.
Baadhi ya wataalamu wameweza kuelezea chimbuko la ushairi wa Kiswahili kwa kuzingatia mitazamo au nadharia mbili ambazo ni kama ifuatavyo:
Nadharia ya kwanza inadai kuwa; Chimbuko la ushairi wa Kiswahili ulitokana na ujio wa Waarabu.
Na nadharia ya pili inasema kuwa; Chimbuko la ushairi wa Kiswahili ni zao la jamii ya waswahili wenyewe.
Kwa kuanza na nadharia ya kwanza isemayo kuwa chimbuko la ushairi wa Kiswahili ulitokana na ujio wa Waarabu ambayo inaungwa mkono na wataalam mbalimbali kama vile Lyndon Harries (1962) na Knappet (1979)
Kwa kuanza na Lyndon (1962) “Swahili Poetry” anatoa hoja tatu ambazo ni ushairi wa Kiswahili umetokana na Uislamu, ushairi ulianzia kwenye upwa wa kaskazini mwa Kenya hususani Lamu. Na maudhui ya ushairi wa Kiswahili yalitokana na ushairi wa Kiarabu. Utungo wa kwanza wa ushairi andishi wa Kiswahili ni Tambuka, Mwengo bin Athmani (1728)
Ubora wa nadharia hii au mtazamo wa Harries kuhusu chimbuko la ushairi wa Kiswahili ni kwamba umesaidia wengine kuendelea kuchunguza zaidi kuhusu chimbuko la ushairi wa Kiswahili.
Udhaifu wa nadharia hii ni kuwa si kweli kwamba ushairi wa Kiswahili uliletwa na Uislamu bali ulikuwepo hata kabla ya ujio wa Uislamu, kwani ushairi hautenganishwi na jamii husika. Hivyo jamii za waswahili walitumia Nyanja mbalimbali za ushairi katika shughuli zao mbalimbali au shughuli zao za kila siku, kama vile; shughuli za kilimo na ufugaji.
Pia ushairi wa Kiswahili ulianza karne ya 10BK na ushairi wa Kiswahili ulikuwa ukitungwa na kughanwa kwa ghibu bila kuandikwa. Wataalam wengi wanakubaliana kuwa asili ya ushairi wa Kiswahili ni tungo simulizi hasa ngoma na nyimbo.
Udhaifu mwingine katika mtazamo wake wa kusema kuwa ushairi ulianzia pwani ya kaskazini ya Kenya si kweli kwa kuwa waswahili walikuwepo hata sehemu nyingine kama vile Kilwa na Bagamoyo ambapo ushairi wa Kiswahili ulitumika.
Hoja ya kusema ushairi wa Kiswahili ulitokana na Kiarabu haina mashiko kwa kuwa waswahili walikuwepo hata kabla ya waarabu na walikuwa na ushairi wao isipokuwa ujio wao ulileta athari kubwa kwa kuwa ulichanganya na mambo ya dini ya kiislamu na hati.
Knappert (1979) “Four centuries of Swahili verse” anasema; “Ushairi wa Kiswahili ulichipuka kwenye upwa wa Kenya kutokana na nyimbo na ngoma za waswahili na ulianza katika karne ya 17 na pia ni ushairi wa Kiislamu wenye kuchanganya sifa za tungo za kiafrika na za kiajemi.
Ubora wa hoja hii ni kwamba, ni kweli Knappert amekubali kuwa,ushairi wa Kiswahili ulitokana na waswahili wenyewe.
Hata hivyo hoja yake ina udhaifu kwa kuwa ushairi wa Kiswahili ulianza kabla ya karne ya 10 BK na pia amejikita katika maudhui ya mambo mengine kama vile siasa, uchumi na kijamii. Vilevile amechanganya chimbuko la ushairi wa Kiswahili na Uarabu.
Nadharia ya pili inasema kuwa ushairi ni zao la waswahili wenyewe. Nadharia hii imejadiliwa na wataalam mbalimbali akiwemo Shaban Robert, Jumanne Mayoka (1993) na Senkoro, Mulokozi na Sengo.
Jumanne, M. Mayoka (1993) anasema ushairi umetokana na jamii ya wanadamu wenyewe na umesheheneza ukwasi mkubwa wa lugha ambayo imekuwa ikitumika katika hatua zote za kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni katika historia ambayo mwanadamu amepitia, Kwa mfano kuwa msamiati uliotumika tangu enzi za kuishi mapangoni, enzi za uwindaji, ujima, utumwa, vita vya makabila, uvamizi wa wageni, ukoloni na harakati za kupambana na ukoloni hadi kupata uhuru na maendeleo yake.
Ubora wa hoja hii ni kwamba ina mashiko ndani yake kwa sababu, kila jamii ina sanaa yake na ushairi ni moja kati ya sanaa hizo ingawa inaweza ikaathiriwa na sanaa ya jamii nyingine. Pia ushairi umekuwa ukikua na kuendelea kadri jamii inavyokuwa na kuendelea.
Udhaifu wa hoja hii ni kwamba si kweli kuwa katika kipindi hicho ushairi ulikuwa tayari umesheheni ukwasi mkubwa wa lugha, na kama ulikuwa kweli umesheheni huu ukwasi wa lugha alipaswa kutuonesha huo utajiri wa lugha anaouzungumzia katika ushairi.
Senkoro (1988) anasema kuwa ushairi uliibuka pale lugha ilipoanza katika kipindi cha uhayawani (kipindi ambacho mwanadamu alipoanza kupambana na mazingira yake) kwenda katika kipindi cha urazini (maana) ili kumwezesha binadamu na mazingira yake kwa mfano, zana za kazi zilizotumika ziliwafanya waimbe kwa kufuata mdundo wa zana hizo.
Ubora wa hoja hii ni kwamba unathibitisha kuwa chimbuko la ushairi ni waswahili wenyewe, kwani umefanikiwa kueleza kuwa katika jamii yoyote ile maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii huambatana au huenda sambamba na maendeleo ya sanaa mbalimbali ikiwemo ushairi uliotumika katika harakati mbalimbali za maisha ya mwanadamu.
Pamoja na kuwa nadharia hii imeonesha kukubalika na wataalamu mbalimbali kama vile Senkoro, Mayoka na Shekhe Amri Abeid, lakini bado ina mapungufu. Hii ni kwa sababu imeshindwa kuonesha muda maalumu ambapo ushairi wa Kiswahili ulianza na ni wapi ulianza kutumika. Hili ni suala ambalo linaumiza vichwa vya wataalamu mbalimbali hadi hivi sasa, kwani hakuna mtaalamu yoyote aliyefanikiwa kuonesha ni wapi na ni lini ushairi wa Kiswahili ulianza.
Hivyo basi, kutokana  na nadharia hizo mbili tunaungana na nadharia inayosema kuwa, chimbuko la ushairi wa Kiswahili ni zao la waswahili wenyewe, kwa sababu waswahili wana utamaduni wao ambao ulikuwepo kabla ya ujio wa Waarabu. Na waliutumia ushairi huo katika shughuli mbalimbali za kijamii, kwa mfano katika harusi, jando na unyago.

MAREJEO:
Knappert, J. (1979). Four centuries of Swahili Verse. Heinemann. London.
Mayoka, J.K. (1993). Mgogoro wa Ushairi na Diwani ya Mayoka. Ndanda Mission                                             Press.Tanzania.
Mulokozi, M.M. (1996). Fasihi ya Kiswahili.Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam. Dar-es-Salaam.
Senkoro, F.E.M.K. (1987). Ushairi, Nadharia na Tahakiki. DUP. Dar-es-Salaam.
TUKI. (1983). Makala ya Semina ya Kimataifa ya Waandishi wa Kiswahili. (Toleo la III) TUKI.Dar-es-Salaam.
TUKI. (2004). Kamusi ya Kiswahili Sanifu.TUKI.Dar-es-Salaam.

 Maintained by an  ICT consultant and Director of Studies:  IFF YOU NEED HELP PLZ CALLA US VIA 0782 474941 0767 4749411 OR VIST www.kcckibaha.blogspot.com kcckimisha@gmail.com

No comments:

Post a Comment